Home About Press Clubs Multimedia Contact Us Staff Mail

Rais wa UTPC afungua mafunzo kwa waandishi wa habari Dodoma

29-Nov-19

Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC), Bwana Deo Nsokolo, amefungua rasmi mafunzo ya uandishi wa habari za Vijijini kwa wanachama wa Klabu za Waandishi wa habari nchini yaliyofanyika mkoani Dodoma.

Akifungua mafunzo hayo, Bwana Deo Nsokolo  amesema kwamba mafunzo wanayokwenda kupewa waandishi hawa ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za UTPC katika Mpango Mkakati wake 2016 - 2020, ambao unaelekea mwishoni.

Alisema kwamba UTPC inapenda kuona mafunzo haya yanafanyiwa kazi kwa waandishi wa habari kuandika habari ambazo zitachangia maendeleo ya mikoa husika  lakini pia kupata waandishi wa habari wabobezi kwenye eneo wanalopata mafunzo.

Aliongeza kwamba UTPC inapenda kuona katika mafunzo haya kila mtu anapata nafasi ya kushiriki lakini pia kuwepo na mchanganyiko wa wanachama na viongozi wa klabu na ndio maana mafunzo haya yanatolewa kwa utaratibu wa wanachama kuomba na kuchaguliwa.

Akijibu swali la Bwana Adam Malima, kuhusu nafasi ya UTPC katika kutetea ajira za waandishi wa habari na mikataba yao, Rais wa UTPC alisema kwamba suala la ajira ni tatizo kwenye tasnia ya habari, ila zipo jitihada ambazo zinafanywa na UTPC kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kihabari ili kwa pamoja kutatua tatizo hili.

“Jambo la kufanya ni kwamba wamiliki wa vyombo vya habari wawathamini waandishi wao kwa kuwapa mikataba na kuwalipa vizuri ili kuboresha tasnia ya habari lakini pia kwa kufanya hivyo maadili ya uandishi wa habari yatazingatiwa kwa kuwa kila mwandishi atakuwa na uhakika wa ujira wake” -  Alisema Deo Nsokolo

Akizungumzia suala la maadili kwa wandishi wahabari, Bwana Deo Nsokolo aliwataka waandishi wa habari kutotumia tasnia ya habari kwa kutekeleza uovu wao.

“Msitumie tasnia ya habari kufanya uovu au kujificha nyuma ya uandishi wa habari kwa uovu wenu mkitegemea UTPC itawatetea, UTPC haitetei uandishi wa habari usiongizatia maadili na taaluma Kila mwandishi afanye kazi yake kwa kufuata maadili ya uandishi wa habari.” – Deo Nsokolo 

Pamoja na mambo mengine, Rais alisema kwamba, vyombo vya habari vimejaa hofu kubwa na waandishi wamekosa nguvu ya kuendelea kufanya kazi kwa uthubutu.

Bwana Nsokolo alizungumia huduma zinazotolewa na UTPC kwa Klabu za Waandishi wa habari,  alisema kwamba UTPC inafanya mambo mengi ukiachilia mbali mafunzo kwa waandishi wa habari. Alizitaja huduma hizo kamna vile kodi ya pango kwa Press Clubs zote, Internet, Maji na Umeme, vifaa kama vile compyuta na Kamera ambavyo vinapelekwa moja kwa moja kwenye klabu.

“Kwenye klabu zenu mnapashwa kuwa na intaneti wakati wote, lakini pia Klabu za waandishi wa habari zinapashwa kuwa ni ofisi zenye hadhi kwa kuwa UTPC inalipa kodi za ofisi hizo”

Rais alimaliza kwa kusema kwamba, mwaka 2020 ni ukomo wa ungozi kwa viongozi wa klabu hivyo UTPC na klabu zake wanategemea kufanya uchaguzi wa viongozi wake kwa mwaka huo. Aliwatia moyo washiriki hao kwamba wasisite kushika nafasi ya uongozi kwenye klabu au katika Bodi ya Wagurugenzi ya UTPC.

“Ikifika wakati wa uchaguzi hakikisheni mnachagua viongozi wazuri wa klabu zenu ili klabu zenu ziendelee kusimama” – Alisema Deo

Mafunzo mengine yaliyofanyika mkoani Dodoma katika wiki hiyo ni Mafunzo ya uandishi wa habari za Mazingira na mafunzo ya uandishi wa habari za Jinsia.