SERIKALI YAANZA KUJENGA MAHUSIANO ENDELEVU NA WAANDISHI WA HABARI

Mkurugenzi wa idara ya habari Maelezo na msemaji mkuu wa Serikali Ndg. Gerson Msigwa amesema Serikali imeanza kujenga mahusiano endelevu na waandishi wa habari na taasisi zinazomia waandishi wa habari nchini, hatua ambayo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi.
Msigwa ameyasema hayo alipokutana na Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa habari nchini UTPC Deogratius Nsokolo mjini Singida.
Msigwa amesema Serikali inatambua mchango wa waandishi wa habari na Press Club nchini katika kusimamia maadili na kusaidia maendeleo katika mikoa mbalimbali na ndio maana ameamua kuweka utaratibu wa kutoa taarifa za Serikali Kwa kukutana na waandishi katika mikoa mbalimbali.
Amesema hatua hiyo inawapa fursa waandishi kuuliza juu ya mkoa wao na Taifa.
"Nimemualika Rais wa UTPC hapa Singida ili kuonyesha azma ya serikali kuwathamini na kuwatumia wandishi wa habari katika mikoa yote kueleza masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali lakini Serikali kupata mrejesho kupitia kwao Kwa kuwa ndio wapo karibu zaidi na wananchi" alisema Msigwa.
Kwa upande wake Rais wa muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania Deogratius Nsokolo alimshukuru Msemaji mkuu wa Serikali Kwa kutambua mchango wa UTPC na Press Clubs nchini pamoja na taasisi nyingine za habari nchini katika maendeleo ya nchi.
Alisema Press Clubs na UTPC zipo tayari kutoa ushirikiano wa dhati ili kuhakikisha wananchi habari ambazo zitawasaidia kupata maendeleo.
Nsokolo pia alimuomba Msemaji mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi mkuu wa idara ya habari Maelezo kushughulikia changamoto zinazowakabili wanahabari nchini na hasa sheria, mikataba ya ajira na ujira, mambo ambayo ameahidi kiyashughulikia kupitia bodi ya ithibati itakayoundwa hivi karibuni.
Aidha Nsokolo amempongeza Msigwa Kwa ubunifu mbalimbali tangu ateuliwe kushika nyadhifa hizo, ubunifu ambao umefanya wananchi kupata taarifa za Serikali Kwa urahisi na waandishi kupata taarifa mbalimbali kupitia mikutano inayofanyika kila jumapili ya wiki.
Msemaji mkuu wa Serikali katika mkutano wake na waandishi wa habari pamoja na mambo mengine ametoa taarifa kuhusu maendeleo ya utoaji chanjo ya Uviko 19 na kuwataka wananchi kujitokeza kuchanja ili kujikinga na ugonjwa huo hatari.