Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) Mhandisi James Kilaba amewataka waandishi wa habari kote nchini kujiendeleza kielimu ili kukidhi matakwa ya kisheria, kwani TCRA itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa waandishi wote watakaokosa vigezo, lengo likiwa ni kuendelea kuimarisha tasnia ya habari nchini, lakini pia kusimamia maudhui na kuleta mshikamano na amani nchini.
Aliyasema hayo hivi karibuni katika Mkutano wa majadiliano kati ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) na waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mwanza yaliyoandaliwa na Klabu Ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC).
Aliongeza kuwa TCRA itaendelea kuchukua hatua kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa maudhui mitandaoni, ikiwa ni pamoja na kuwa na vitendea kazi vya kisasa na raslimali watu wa kutosha ili kuleta ufanisi kwenye sekta ya mawalisiano.
Pamoja na hayo, Bw. Kilaba alisema kuwa sheria ya habari ya mwaka 2016 inamtaka kila mwandishi kuwa na elimu ya kuanzia ngazi ya “Diploma” ambapo serikali imetoa kipindi cha mpito cha muda wa miaka 5 kitakachondelea hadi tarehe 31 Disemba, 2021, ili kutoa nafasi kwa kila mwandishi kujiendeleza kielimu na kufika ngazi ya Diploma.
Hata hivyo Bw. Kilaba aliwaambia waandishi hao kuwa, TCRA ilitoa kumbusho kwa wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuzingatia matakwa ya sheria na masharti ya leseni za utangazaji kwa kuhakikisha kuwa wanaotangaza katika vyombo vyao wanakuwa na vigezo vya kitaaluma kama waandishi wa habari.
Naye Mkurugenzi wa UTPC Bw. Abubakar Karsan, alitoa wito kwa waandishi wa habari kuhakikisha wanafuata sheria wakati wanatekeleza majukumu yao ya kila siku.
Pamoja na wito huo, Bw. Karsan alitoa shukrani kwa Mkurugenzi wa TCRA kwa kukubali kushiriki kwenye mkutano huo maalumu kwa waandishi wa habari mkoa wa Mwanza.
Pia aliongeza kuwa, mwaka 2020 UTPC imeandaa mpango maalumu wa kuziwezesha klabu zote 28 nchini kusajili blog zao ili iwe rahisi kuchapisha habari nyingi za mkoa husika na kusaidia kuleta maendeleo ya Mkoa na nchi kwa ujumla.