UTPC YATOA VIFAA VYA KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UGONJWA WA COVID19 KWA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA.

Umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC), umeanza kutoa vifaa mbalimbali vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID19 kwa klabu za waandishi wa habari na wanachama wake nchini kote.

Maamuzi haya yamefikiwa ili kuendelea kutoa ulinzi kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa mstari wa mbele kutafuta na kutoa habari kwa wadau wote nchini hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya ugongwa wa COVID19.

 

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na Barakoa, vitakasa mikono, ndoo za kuwekea maji, karatasi laini (Tishu), glavu (gloves) na vingingenevyo. Vifaa hivi vimetolewa kwa mwandishi mmoja mmoja na vingine vimetolewa kwa ajili ya ofisi za klabu.

 

Pamoja na mambo mengine, UTPC inapenda kutoa shukrani za dhati kwa wadau mbalimbali ambao wameendelea kuzisaidia klabu za waandishi habari kwa kutoa vifaa mbalimbali vya kujilinda na maambukizi haya ugonjwa wa COVID19. UTPC inathamini sana mchango wa wadau wote walioshiriki kikamilifu kuhakikisha mwandishi wa habari anakuwa salama ili aendelee kuuhabarisha umma katika kipindi hiki kigumu ambapo jamii inahitaji taarifa sahihi ili kuongeza uelewa na usalama wao.

 

Hata hivyo UTPC inapenda kuwasisitiza waandishi wa habari kuendelea kuchukua tahadhari za kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID19 kwa kufuata masharti yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo Wizara ya Afya na WHO.