MWANZA PRESS CLUB YAENDESHA MDAHALO

Mwanza Press Club leo imeendesha mdahalo kuhusu Maadili ya Uandishi wa habari, Uhuru wa Kujieleza na Haki ya kupata taaarifa, mdahalo ambao ulifunguliwa rasmi na Afisa Habari kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. Abel Ngapemba ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. Mhandisi Robert Gabriel.
Mdahalo huu umejumuisha waandishi wa habari kutoka Klabu za Waandishi wa Habari za mikoa ya Mwanza, Geita, Mara na Simiyu.
Pamoja na ushiriki huo kutoka Press Clubs, pia Mdahalo huu ulijumuisha wadau muhimu wa habari kutoka ofisi ya Mkuu ya Mkoa wa Mwanza ambayo iliwakilishwa na Afisa Habari wake Bw. Abel Ngapemba, kutoka TCRA alikuwepo Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Ziwa Bw. Francis Mihayo, kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, iliwakilishwa na Inspector Mwita Robert na Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Nyamagana (Mh. Stanslaus Mabula) iliwakilishwa na Bi. Florah Magabe.
Pamoja na kujadili mambo mengi kuhusu Maadili ya Uandishi wa Habari, Haki ya kupata taarifa na Uhuru wa Kujieleza, wajumbe wa mdahalo huu wamekubaliana kuendelea kufanya mambo makubwa matano kama maazimio ya Mdahalo huo.
1. Kuitisha Mkutano mkubwa wa wadau na waandishi wa habari kanda ya ziwa kujadili changamoto zinazoikabili tasnia ya habari na utatuzi wake. Mkutano huu utaitishwa kwa ushirikiano wa TCRA kanda ya ziwa, UTPC na MPC.
2. Kuandaa utaratibu wa kuendelea kujengeana uwezo kwa kutumia midahalo na mafunzo kwa ushirikiano wa waandishi na wadau wa habari kwenye maeneo mtambuka ambayo yanawakutanisha wadau na waandishi wa habari mara kwa mara.
3. Kuendelea kutoa maoni ya kuboresha sheria zinazogusa tasnia ya habari nchini, mfano EPOCA, MSA na Statistics Act
4. Kuimarisha mahusiano kati ya waandishi wa habari na wadau wa habari hasa hasa taasisi za serikali kwa kutengeneza WhatsApp Group ili kuongeza wigo wa kupeana taarifa mara kwa mara.
5. Kufanya tafiti na kutoa machapisho yatakayoendelea kuongeza uelewa na kuhamisha masuala mazima ya Uhuru wa Kujieleza, Uhuru wa kutoa na kupata taarifa na maadili ya uandishi wa habari.
Mdahalo huu ni utekelezaji wa moja ya shughuli zilizomo kwenye mradi wa ushirikiano kati ya shirika la IMS (International Media Support) na UTPC.
Shughuli nyingine ni mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu ulinzi na usalama wa mwandishi wa habari, midahalo ya ulinzi na usalama kwa mwandishi wa habari, kuandaa kanuni za maadili ya uandishi wa habari na ufwatiliaji wa madhila kwenye tasnia ya habari.