Mchakato wa kukusanya maoni kuhusu uandaaji wa kanuni za maadili ya uandishi wa habari wakiwemo watoa maudhui mtandaoni, umemalizika leo mkoani Mwanza kwa Mwanza Press Club kushiriki kama klabu ya mwisho kuandaa mkutano huu.
Tangu mchakato huu umeanza, klabu za waandishi wa habari 28 zimeshirikishwa kwenye mchakato huu kwa nyakati tofauti.
Klabu za Waandishi wa Habari ambazo zilipewa nafasi ya kuandaa mikutano hii na kutoa nafasi kwa klabu za jirani kutuma wawakilishi wao ni Dar es Salaam, Arusha, Zanzibar, Kigoma, Iringa, Dodoma, Mtwara na Mwanza.
Mikutano hii ni moja ya utekelezaji wa shughuli zilizopo kwenye mradi wa ushirikiano kati ya UTPC na IMS (International Media Support) ambao mradi huu umelenga kuzijengea uwezo taasisi za kihabari kushiriki katika ushawishi kuhusu uhuru wa habari na uhuru wa wananchi kupata taarifa.
Mradi huu unaendeshwa na shirika la International Media Support la nchini Denmark, ambao wamefadhiliwa na Umoja wa Ulaya (European Union).