UTPC imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha aliyekuwa mfanyakazi wa UTPC, ndugu Jacob Njayeje Kambili, kilichotokea katika hospitali ya Bugando baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Jacob Ngayeje Kambili alizaliwa tarehe 22 Oktoba 1953 na kufariki dunia tarehe 29 Julai 2020 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Marehemu alisumbuliwa sana ugonjwa wa Tezi Dume ambao ulimfanya kushindwa kuendelea kufanya kazi na UTPC na kuamua kustaafu rasmi mwaka 2018.
Marehemu Jacob Njayeje Kambili alikuwa ni mwandishi wa habari mkongwe aliyefanya kazi kwa umahiri na kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma yake. Marehemu alifanya kazi na UTPC kwa kipindi kisichopungua miaka 7 na kabla ya hapo alifanya kazi na klabu ya waandishi wa habari Mwanza (Mwanza Press Club) akiwa kama Katibu wa klabu hiyo huku akiendelea na taaluma yake ya uandishi wa habari ambapo alifanya kazi kwenye vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini ikiwemo Gazeti la Daily News.
Marehemu Jacob Ngayeje Kambili alikuwa mcha Mungu mwenye upendo wa dhati kwa wafanyakazi wenzake lakini pia mkweli na mcheshi wakati wote.
Kwa niaba ya wanahabari wote Tanzania, UTPC inapenda kutoa pole kwa msiba huu mzito ambao umewagusa watu wengi ambao walifanya kazi na marehemu kwenye tasnia ya habari.
Mungu ailaze roho ya marehemu malaha pema peponi amina.