WAANDISHI WA HABARI WAPEWA MAFUNZO YA ULINZI NA USALAMA

Mafunzo ya siku mbili kuhusu Ulinzi na Usalama kwa Mwandishi wa Habari, yamemalizika leo mkoani Dodoma ikiwa ni awamu ya pili kufanyika kwa mafunzo haya.
Washiriki 20 kutoka klabu za waandishi wa habari nchini wameshiriki mafunzo haya ambayo yameongozwa na Mwandishi mbobezi Bw. Neville Meena kutoka Jukwaa la Wahariri.
Akifunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Dodoma na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya UTPC Bw. Mussa Yusuph amewataka waandishi waliopata mafunzo haya kuzingatia kile walichofundishwa kwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufahamu mipaka ya kazi yao ili kulinda maisha yao kwakuwa waandishi wanapopata matatizo na kushindwa kufanya kazi, inayoathirika zaidi ni jamii ambayo inamtegemea Mwandishi wa Habari kupata taarifa sahihi ili mwisho wa siku jamii hiyo ifanye maamuzi sahihi.
Pamoja na mambo mengine Bw. Mussa aliwashukuru wafadhili wa mradi huu ambao ni shirika la IMS kutoka nchini Denmark ambao wameiamini taasisi ya UTPC na kuamua kufanya nayo kazi.
Mpaka kufikia mwisho wa mradi huu, waandishi wa Habari 100 wanatakiwa wawe wameshapata mafunzo haya ya Ulinzi na Usalama.