- Jan 14,2022
- General
WAMILIKI VYOMBO VYA HABARI WATAKIWA KUWALIPA WAANDISHI STAHIKI ZAO
Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania wametakiwa kuwalipa Waaandishi wa Habari stahiki zao kwani ni haki yao ya kimsingi na kisheria.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Bwana Abubakar Karsan alipokuwa akihutubia maelfu ya waombolezaji waliohudhuria kuaga miili ya waandishi wa habari watano na dereva mmoja katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Ameongeza kuwa baadhi ya Waandishi wa Habari hawajalipwa mishahara yao kwa takribani miaka miwili, na kuwa hii ni kwa sababu hakuna uwanja mzuri wa sheria zinazolinda maslahi ya Waandishi wa Habari.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye ameagiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi juu ya ajali zinazotokea zikihusisha magari wanayopanda Waandishi wa Habari katika misafara ya viongozi wa Serikali ili kuweka mikakati ya kudhibiti na kuzuia ajali hizo.
Akijibu hoja iliyotolewa na Mkurugenzi wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Bwana Abubakar Karsan,Waziri Nape amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuewalipa marehemu malimbikizo ya stahiki zao ndani ya siku saba na kisha warepoti kwa Mkuu wa Mkoa wakiwa na vielelezo vya malipo.